Tuesday, 31 May 2016

Stars yawaandalia kipigo Mafarao Dar

Mshambuliaji wa timu ya soka ya Taifa Tanzania, ‘Taifa Stars’, Elias Maguli (kulia) akichuana na David Odhiambo wa Kenya ‘Harambee Stars’ wakati wa mchezo wa kirafiki wa Kimataifa baina ya timu hizo uliofanyika Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi, Kenya juzi. Timu hizo zilifungana 1-1. (Na Mpigapicha Wetu).
TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imerejea nchini kutoka Nairobi, Kenya, ambako mwishoni mwa wiki ilicheza na wenyeji wao, timu ya taifa ya nchi hiyo `Harambee Stars’ na kutoka nao sare ya 1-1 katika mchezo mkali wa kirafiki kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi.
Lakini baada ya kurejea jana asubuhi, timu hiyo imekwenda moja kwa moja kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku kocha mkuu, Charles Boniface Mkwasa akiapa `Misri hawatatoka’.
“Najua Misri wanatufuatilia. Na hata Kenya kwa siku zote tatu walikuwepo. Najua Misri wanahitaji hata sare ili wafuzu kwa fainali hizi, lakini hawataipata Tanzania,” alisema Mkwasa kwa msisitizo. Stars na Misri zinakutana katika mchezo wa marudiano wa kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka kesho huko Gabon.
Katika mchezo wa kwanza mwishoni mwa mwaka jana, Misri wakiwa nyumbani walishinda 3-0. Mkwasa alisema jana kuwa, kwa jinsi msimamo ulivyo kwa sasa, Misri wanaifuatilia Stars na walikuwepo Nairobi kushuhudia mchezo wao ili wapate mbinu za kushinda kirahisi, lakini akaapa hilo walisahau.
Alisema pamoja na kuifanyia ushushushu Stars, Misri haitakuwa na jeuri ya kuifunga Tanzania jijini Dar es Salaam, akisema ana uhakika vijana wake watajitahidi ili kupata matokeo mazuri baada ya Jumapili kufanya vema dhidi ya Harambee Stars.
Wakati Misri wana pointi saba, Taifa Stars ina pointi moja katika kundi lao la G, hivyo sare yoyote kwa Misri itawahakikishia kufuzu kwa fainali, lakini ikifungwa itaweka hai matumaini ya Tanzania kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980.
Hata hivyo, itawezekana endapo itashinda ugenini dhidi ya Nigeria katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
“Kama nilivyosema, Misri wanahitaji pointi moja. Lakini sisi tunahitaji pointi tatu. Mchezo wa Kenya unatosha kuona mapungufu. Maana ilikuwa mechi ngumu iliyojaa nyota wote wa Kenya ambao ni professionals, lakini mimi nilikuwa na local based players na matokeo yamekuwa hayo.”
Mkwasa alisema ana taarifa namna ambavyo Misri wanaifuatilia Taifa Stars hususani ukusanyaji wa video kwa ajili ya kuona aina ya soka la Tanzania, ambapo alisisitiza kuwa kamwe hawatafanikiwa. Kwa mara ya mwisho Tanzania ilifuzu kwa fainali hizo za Afrika mwaka 1980 wakati Mkwasa akiwa miongoni mwa wachezaji wa kikosi hicho.
Mkwasa alipongeza Shirikisho la Soka Kenya (FKF), kwa kuandaa mchezo huo angalau kwa asilimia 70 kwa kushirikiana na Tanzania iliyojazia gharama sambamba na vijana wake kwa kucheza kwa kujituma licha ya kuwakosa nyota wake wa kulipwa.
Taifa Stars ilicheza mchezo huo bila ya nyota wake wa kimataifa, Mbwana Samata anayeichezea timu ya Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya DRC.
Naye Mwinyi Kazimoto aliyekuwa nahodha wa Stars dhidi ya Kenya, alisema mchezo dhidi ya Kenya umewapa picha halisi ya utayari wao kuwavaa Misri na kwamba, wako tayari kwa hilo.
Katika mchezo huo, nahodha wa Kenya, Victor Wanyama anayeichezea klabu ya Southampton ya Ligi Kuu ya England, alielezea kushangazwa na ubora wa kikosi cha Stars kilichoonesha soka maridadi licha ya kutokuwa na nyota wake wanaocheza soka ya kulipwa nje ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment