Monday, 23 May 2016

Rais Fifa atia ubani ubingwa wa Yanga


Kikosi cha Yanga.







RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ameipongeza timu ya soka Yanga ya Dar es Salaam, kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2015/16. Yanga imetwaa ubingwa huo kwa msimu wa pili mfululizo, lakini ikiwa ni mara ya 26 tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara mwaka 1965.
Katika salamu zake, kupitia barua yake ya Mei 18, 2016 kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, Infantino ameelezea ubingwa wa Yanga kwamba umetokana na kazi kubwa inayofanywa na uongozi wa timu hiyo, makocha, wachezaji pamoja na mashabiki.
“Yanga ndiyo mabingwa wa Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Yanga na timu nzima isiyoshindika kwa mafanikio haya makubwa. Taji la Yanga ni matokeo ya mshikamano ulioko ndani ya timu hiyo,” alisema Infantino katika barua hiyo yenye kichwa cha habari kinachosema: Salamu za Pongezi kwa Yanga.
Amesema pongezi zake ziende kwa uongozi wa klabu, makocha na benchi zima la ufundi, wachezaji, madaktari na mashabiki wa Yanga. Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikwisha kuipongeza Yanga ambayo imepewa Kombe na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji na kwa sasa wanasubiri zawadi ya fedha Sh 81,345,723.

No comments:

Post a Comment