BAADA ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kuingia bungeni akiwa amelewa, Ofisi ya Bunge imesema hakuna kanuni inayotaka wabunge wapimwe ulevi na haioni sababu ya kuwapima kwa sababu ni watu wazima.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema, Kanuni za Kudumu za Bunge hazina kanuni inayozungumzia suala la ulevi. Akizungumza na gazeti hili, Joel alisema lakini katika mabunge mbalimbali duniani wameweka taratibu za kimaadili zinazowaongoza wabunge.
“Kwa kweli hakuna sababu ya kupima wabunge ulevi kwa sababu hawa ni watu wazima wanaojitambua. Kanuni za Bunge hazina kipengele kinachozungumzia suala la ulevi. “Lakini wabunge wanaandaa kanuni zao za maadili, humo ndio wataweka mambo yao ya nini cha kuzungumzwa na wabunge, kusema wenzao na mengineyo.
Ni Code of Conduct kwa wabunge wenyewe,” alisema Joel. Alisema hilo linafanyika katika mabunge mbalimbali duniani kwa kuwa na taratibu zao za kimaadili zinazowaongoza. Kaimu Katibu wa Bunge alisema hayo, baada ya kuulizwa na gazeti hili kuhusu hoja iliyoibuka baada ya kutenguliwa kwa uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kitwanga kwa kuingia na kujibu swali bungeni akiwa amelewa.
Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu alisema Rais Magufuli alitengua uteuzi huo kutokana na kitendo cha Kitwanga kuingia bungeni na kujibu swali linaloihusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwa amelewa.
Hoja ya kutaka kuwapo kwa kipimo cha ulevi kwa wabunge kabla ya kuingia bungeni, ilitanda katika mijadala nchini juzi baada ya Kitwanga kufukuzwa. Mbunge wa Arusha Mjini, Gobless Lema ambaye pia ni Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ni mmoja wa waliounga mkono hoja hiyo.
Lema alikaririwa akisema katika taarifa ya habari ya kituo cha televisheni cha ITV juzi usiku, akipendekeza sasa kuwapo kwa kipimo cha ulevi kwa wabunge kabla ya kuingia ukumbini, akisema kitasaidia kuondoa wabunge na mawaziri walevi.
Katika taarifa yake saa chache baada ya kutimuliwa Kitwanga, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema uamuzi uliofanywa na Dk Magufuli umefuata kanuni za utumishi wa umma ambao unakataza mtumishi kulewa akiwa kazini.
“Zipo sheria za utumishi ambazo mtumishi hatakiwi kunywa pombe na wala hapaswi kulewa akiwa kazini… mtumishi anapaswa kuwa na akili timamu inayokuwezesha kufanya kazi za serikali,” alisema Majaliwa akijibu swali la mwandishi wa TBC1 aliyetaka kujua ukweli wa taarifa za kutimuliwa Kitwanga.
“Ni kweli Mheshimiwa Rais, Dk John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Charles Kitwanga kuanzia leo tarehe 20 Mei, 2016 baada ya kuonekana amelewa wakati wa kazi. Na hili lilibainika pale alipokuwa akijibu maswali ya wizara yake leo asubuhi,” alisema Waziri Mkuu.
Kwa utaratibu wa sasa, wabunge na wageni wote wanaoingia ndani ya viwanja vya Bunge, hukaguliwa kwa mashine maalumu, ambazo huangalia kama mtu amebeba vitu visivyokubalika, kama silaha, visu na vingine vyenye ncha kali.
No comments:
Post a Comment