Tuesday, 31 May 2016

Majambazi wauawa wakikimbizwa na polisi

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Simon Sirro

WATU wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wameuawa na mwingine mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kujihusisha na ujambazi jijini Dar es Salaam.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema tukio hilo lilitokea Mei 28 mwaka huu baada ya polisi kupata taarifa kuwa maeneo ya Mburahati kuna majambazi watatu, ambao walikuwa wanafukuzwa na kundi la bodaboda huku wakifyatua risasi.

Sirro alisema katika ufuatiliaji askari walifika katika eneo hilo na kukuta jambazi mmoja akishambuliwa na wananchi baada ya silaha aliyokuwa akiitumia kuishiwa risasi.

Jambazi huyo alikutwa na silaha moja, bastola LLA yenye namba 649440. Alisema majambazi wengine wawili, walikimbia wakiwa na bodaboda yenye namba za usajili MC 444 BFY.

Polisi waliwakimbiza wakishirikiana na madereva bodaboda hadi kufika katika eneo la Kisukuru, ambako majambazi hao walianguka na kuangusha bastola yao aina ya Chinese Star, ndipo wananchi walianza kuwashambulia kwa mawe na fimbo.

Aliongeza kuwa majambazi hao, walishambuliwa baada ya muda mfupi walifariki dunia huku mwingine alifanikiwa kukimbia na begi dogo jeusi lililokuwa na fedha.

Sirro alisema awali majambazi hao, walikuwa watatu wakiwa kwenye pikipiki maeneo ya Buguruni, ambapo walifanya tukio la uporaji wa Sh 500,000 mali ya Mushi Bakari, aliyekuwa na gari namba T 786 CZI Toyota IST ambaye walimjeruhi mkono wa kulia.

Katika tukio jingine, jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mtu mmoja anayetuhumiwa kuwa jambazi huko Temeke akiwa na bastola Glock P241 yenye namba NK 172374 ikiwa na risasi 14 ndani ya magazini.
Alisema jambazi huyo alikamatwa baada ya kufanya tukio la uporaji maeneo ya Chang’ombe Maduka Mawili ya Tigo Pesa akiwa na mwenzake, ambapo walikimbia kwa kutumia pikipiki.

No comments:

Post a Comment