Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi
KUSHUKA kwa bei ya umeme kwa wateja wa kada mbalimbali wa nishati
hiyo na kuondolewa kwa tozo ya huduma ya kila mwezi ya Sh 5,520 kwa kila
mteja wa nyumbani, kumerudisha kwa Watanzania zaidi ya Sh bilioni 69,
iliyokuwa ikienda katika Shirika la Umeme (Tanesco).
Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Felix
Ngamlagosi, amesema hayo mwishoni mwa wiki, alipokutana na Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC).
Kwa mujibu wa Ngamlagosi, kufutwa tu kwa tozo ya kila mwezi ya huduma
kwa wateja wa majumbani ambayo ilikuwa Sh 5,520, ambayo ni mbali na
punguzo la bei kwa kada mbalimbali za wateja, kumewarejeshea Watanzania
Sh bilioni 69, ambazo hapo awali zilikuwa zikienda Tanesco.
Alipoulizwa iwapo hatua hiyo ya kupunguza bei ya umeme imetokana na
shinikizo kutoka serikalini na kama kutayumbisha shirika hilo muhimu kwa
uchumi wa nchi. Ngamlagosi alisema, kwanza maombi ya kushusha bei hiyo
yametoka Tanesco.
“Sisi tumepokea barua kutoka Tanesco ikituomba suala la kushusha bei
ya umeme na sio kwamba walilazimishwa na Serikali na sisi tuliwahoji
sana, kama wataweza kujiendesha, baada ya kuridhika na maelezo yao na
uchunguzi wetu, ndipo tukakubali,” alisema Ngamlagosi.
Faida ya gesi Akifafanua matokeo ya uchunguzi uliochangia wakubali
kushushwa kwa bei hiyo, Ngamlagosi alisema walibaini ukweli kwamba hivi
sasa mitambo ya kuzalisha umeme huo unaouzwa na Tanesco, mingi haitumii
tena mafuta, bali inatumia gesi asilia inayochimbwa hapa nchini
Umeme wa mafuta ulikuwa ghali kwa kuwa kwanza yananunuliwa kwa fedha
za kigeni na hivyo kuporomoka kwa Shilingi, kuliongeza gharama za
ununuzi na pia bei yake kimataifa, ina tabia ya kubadilikabadilika,
tofauti na gesi inayochimbwa nchini.
Capacity Charge Ngamlagosi alisema mbali na faida ya kutumia umeme
unaotokana na gesi, ambao kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli
(TPDC), karibu asilimia 70 ya umeme wote kwa sasa ni wa gesi, pia
walibaini mitambo yote ya kufua umeme wa dharura imeondolewa.
“Ni kweli Tanesco hivi sasa wanatumia kiasi kidogo cha mafuta na
mitambo yote ya dharura haitumiki tena, pia vyanzo vya nishati
vimeongezeka na vingi ni vya uhakika na hakuna kampuni ya dharura ya
muda mfupi inayolipwa tozo ya uwezo wa mtambo (capacity charge),”
alisema Ngamlagosi.
Tozo hiyo ya uwezo wa mtambo, ambayo ilikuwa ikitozwa katika mitambo
mingi ya ufuaji umeme wa dharura, iliongeza gharama kwa kuwa hata kama
mtambo hauzalishi au umezimwa kabisa, tozo hiyo ilikuwa ikilipwa kwa
siku kwa mabilioni ya Shilingi.
Kutokana na faida hizo, ikiwemo kujaa kwa mabwawa ya kufua umeme wa
maji, Ngamlagosi alisema punguzo hilo si hasara kwa sababu unafuu wa
uzalishaji nishati hiyo nao umeongezeka.
Wafanyabiashara Wakizungumza na gazeti hili jana, wananchi wa kada
mbalimbali nchini wakiwemo wasomi na wanasiasa, wamepongeza Serikali kwa
kushusha bei ya umeme na kueleza ni mwanzo mzuri wa wananchi kuanza
kufaidi kukua kwa uchumi, huku wakitaka wenye viwanda na wafanyabiashara
waangalie namna ya kushusha bei za bidhaa na huduma.
Walisema kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakipata maumivu kutokana
na umeme kuwa ghali, jambo lililofanya wengi kutomudu gharama zake
wakiwemo wa mijini na vijijini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alipongeza
Tanesco, Ewura na Serikali kwa punguzo hilo kwani Watanzania wanaanza
kufaidi uzalishaji wa umeme kwa gesi asilia inayopatikana nchini na siyo
mafuta yaliyokuwa ya gharama kubwa.
Alisema nia ni kumpunguzia mlaji gharama za maisha, kama ilivyo lengo
la Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo
kwa gharama nafuu. “Kutokana na kupungua gharama hii ya umeme hakika na
wazalishaji viwandani watakuwa wamepunguziwa gharama, hivyo ni wakati wa
kufikiria kupunguza gharama za bidhaa zao ili kuendelea kumpatia
mwananchi wa kawaida unafuu wa maisha,”alisisitiza.
Dk Banna alisema ni dhahiri kuwa uchumi wa nchi ulikuwa ukikua katika
vitabu tu huku wananchi wakishindwa kuona manufaa yake lakini sasa
wananchi wameanza kufaidi ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuwa na umeme wa
uhakika na nafuu. Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian
Mukoba alisema suala la kupungua bei ya umeme ni zuri na linadhihirisha
kuwa nchi imepata Rais anayejali wananchi wake.