Yanga iliifunga Mwadui FC ya Shinyanga mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Azam FC ilifunga Mtibwa Sugar bao 1-0 Uwanja wa Manungu, Turiani.
Azam imemaliza mechi zake za viporo, ambapo imecheza mechi 24 ikiwa na pointi 55 ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga iliyocheza mechi 23 ikiwa na pointi 56.
Yanga itamaliza mechi yake ya viporo Jumamosi dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ndiyo inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 24.
Mashabiki wa Yanga ilibidi wasubiri hadi dakika ya 86 kushangilia kwa nguvu bao la pili lililowahakikishia ushindi, mfungaji akiwa Haruna Niyonzima, baada ya kumalizia mpira uliookolewa na mabeki wa Mwadui.
Kabla ya bao hilo, Mwadui ilipata pigo baada ya Iddy Mobby kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Donald Ngoma.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tatu mfungaji akiwa Simon Msuva akiunganisha kwa kichwa krosi ya Oscar Joshua.
Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana kwani dakika ya 13 Mwadui ilisawazisha mfungaji akiwa Kelvin Kabati aliyetumia vyema makosa ya mabeki wa Yanga waliojichanganya.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini umakini wa washambuliaji ulikuwa kikwazo kila walipoingia katika eneo la hatari.
Katika mchezo wa Mtibwa Sugar, washindi walipata bao hilo pekee mfungaji akiwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco.
Azam ingeweza kupata mabao zaidi, lakini washambuliaji wake walishikwa na kigugumizi kila walipokaribia lango la wapinzani wao, hali ambayo pia iliikuta Mtibwa Sugar.
Matokeo hayo yameifanya Mtibwa Sugar ibaki nafasi ya nne ikiwa na pointi 34.
No comments:
Post a Comment