Thursday, 14 April 2016

Kashilillah afafanua fedha za madawati


Katibu wa Bunge Thomas Kashilila.


KATIBU wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah amesema uamuzi wa Bunge kupeleka fedha Ikulu hautakuwa na athari zozote za uendeshaji wa shughuli za taasisi hizo, kama inavyopotoshwa kupitia mitandao ya kijamii.
Aidha, ameelezea kusitikishwa na taarifa hizo zilizoanza kusambazwa siku chache baada ya Bunge kukabidhi hundi ya Sh bilioni 6 kwa Rais John Magufuli ambazo zimepatikana baada ya Bunge kubana matumizi yake.
Aliyasema hayo jana alipokuwa anazungumzia uamuzi wa kuzipeleka fedha hizo Ikulu kama hautakuwa na athari kwenye bajeti ya Bunge hususan kwenye malipo ya posho na mishahara ya wabunge.
Tayari katika baadhi ya mitandao ya kijamii zipo taarifa zinazodai kuwa ofisi ya Bunge imefikia uamuzi wa kupeleka mabilioni hayo ya fedha Ikulu wakati baadhi ya wabunge wakiwa hawajalipwa posho zao na Bunge lenyewe likiwa linakabiliwa na ukata.
Akizungumzia taarifa hizo, Dk Kashilillah alisema ni taarifa potofu kwa sababu fedha zilizowasilishwa kwa Rais Magufuli ni zile ambazo hazikutumiwa na Bunge kati ya Julai na Oktoba mwaka jana, baada ya kuvunjwa kupisha uchaguzi mkuu.
“Huwa ninapata shida kuzungumzia mambo ya kuokota okota, tulipokuwa tunamkabidhi Rais hizo fedha tulieleza na kama kuna mtu anataka taarifa anapaswa kuuliza mamlaka husika siyo kusambaza uongo.
Ni kweli kwamba tumejibana sana kuokoa fedha hizo lakini pamoja na kujibana huko hizi fedha ni za Bunge la 10 ambalo halikufanya kazi kati ya Julai hadi Oktoba mwaka jana.
“Jumla ya fedha tulizookoa ni Sh bilioni 20, lakini sehemu nyingine za fedha hizo tulitumia kulipa gharama za wabunge wapya kama unavyojua idadi ya wabunge sasa imeongezeka pamoja na shughuli nyingine za Bunge. Zilizobaki zilikuwa lazima zirudi, ndiyo utaratibu ulivyo,” alisema Dk Kashalillah.

No comments:

Post a Comment