Wednesday, 13 April 2016

Mabalozi watatu wakabidhi hati za utambulisho kwa Rais




Rais Dk John Magufuli.


RAIS John Magufuli amepokea hati za utambulisho za mabalozi watatu wanaoziwakilisha nchini zao hapa nchini. Balozi wa kwanza kukabidhi hati zake za utambulisho ni Carlos Alfonso Puente wa Brazil aliyesema kuwa nchi yake ipo tayari kuimarisha zaidi uhusiano na Tanzania.

Alitaja maeneo ya uzalishaji wa pamba na miwa kuwa ni miongoni mwa yatakayozingatiwa. Kwa upande wake, Rais Magufuli amemhakikishia Balozi Puente kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na nchi yake.

Pia alitaka uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Brazil uimarishwe zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania inazo rasilimali na fursa nyingi zinazoweza kutumika kwa faida ya pande zote mbili.
Mwingine aliyekabidhi hati zake za utambulisho ni Balozi Pavel Rezac wa Jamhuri ya Czech.

Magufuli ameialika Czech kuungana na Tanzania katika juhudi zake za kuendeleza kilimo na kuzalisha umeme kwa kutumia gesi, ambayo mpaka sasa Tanzania imefanikiwa kugundua uwepo wa futi za ujazo zaidi ya trilioni 57.

Rais Magufuli alimuomba Balozi Rezac kumpelekea salamu Rais wa nchi hiyo, Milos Zeman, kumhakikishia kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano ipo tayari kuimarisha zaidi ushirikiano kukuza biashara na uwekezaji na kujenga uhusiano imara zaidi.

Balozi mwingine aliyewasilisha hati ya utambulisho ni Mariano Deng Ngor wa Sudani Kusini ambaye aliwasilisha salamu za Salva Kiir. Alisema, nchi hiyo itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania.

Aliongeza kuwa, wanaheshimu mchango mkubwa unaotolewa na Tanzania katika kutatua mgogoro wa kisiasa nchini mwao. Rais Magufuli alisema, ataendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati yake na Sudan Kusini.

Alitoa mwito kwa taifa hilo changa kufanya biashara moja kwa moja na Tanzania na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambazo sasa idadi ya watu wake imefikia milioni 165.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliagana na Mahadhi Juma Maalim ambaye hivi karibuni alimteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait. Balozi Mahadhi anakwenda kuanzisha Ofisi za Ubalozi nchini Kuwait, ikiwa ni moja ya juhudi za Tanzania kuimarisha na kuongeza ushirikiano na uhusiano wake na nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.

No comments:

Post a Comment