Ushindi huo ni ishara njema kwa klabu ya Yanga ambayo wiki ijayo itaikabili Al Ahly, kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pia kwa timu ya taifa ya wakubwa ‘Taifa Stars’ ambayo mwezi Juni, itaikabili Misri, katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika ‘Afcon’.
Hadi mapumziko Serengeti Boys, inayonolewa na kocha Bakari Shime, ilikuwa mbele kwa bao moja lililofungwa na kiungo Cyprian Benedictor, aliyewalamba chenga mabeki wanne wa Misri na kumtungua kipa Amro Boghdady.
Kipindi cha pili Misri walionekana kuja juu baada ya kufanya mabadiliko kwa kuwaingiza Mahmud Mohamed na Mohamed Hegaze, kuchukua nafasi za Mohamed Elsayed na Walid Ataia na jitihada zao zilizaa matunda dakika 85 baada ya Diaa Wahed kuisawazishia timu yake kwa shuti kali.
Kuingia kwa bao hilo kuliwazindua Serengeti ambao waliutawala kwa asilimia kubwa mchezo huo na kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Misri, lakini umaliziaji ulikuwa butu.
Wakati mashabiki wakiamini mchezo ungemalizika kwa sare, beki wa kati, Ally Hussein, aliifungia Serengeti Boys, bao la ushindi dakika ya 90, baada ya kupanda mbele na kupokea krosi ya Boko Selemani.
No comments:
Post a Comment