WAKULIMA na wanunuzi wa zao la pamba, katika mikoa ya kanda ya Mangaribi, wamehimizwa kuzingatia ubora wa zao na usafi wa zao hilo, ili liweze kupata soko la uhakika.
Rai hiyo ilitolewa juzi katika Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, na mkaguzi wa viwanda vya pamba mwandamizi, Kisinza Ndimu, kwenye semina ya ubora na usafi wa pamba, kwa wanunuzi wa pamba mbegu ngazi ya vituo, iliyofanyika katika ukumbi wa kiwanda cha kampuni ya Oram LTD mijini Bunda.
Ndimu alisema wakulima na wanunuzi wa zao hilo wamekuwa wakiharibu kwa makusudi ubora na usafi wa zao la pamba, hali ambayo imekuwa ikisababisha thamani yake kushuka kila mwaka.
Alisema wanunuzi wamekuwa wakifanya uharibifu huo kwa asilimia zaidi ya 80 wakati inapofika katika vituo vyao vya kununulia pamba na akayataka makundi yote mawili, pamoja na wadau mbalimbali kuzingatia ubora na usafi wa zao hilo.
“Watu wamekuwa wakiharibu kwa makusudi kabisa ubora na usafi wa zao la pamba, wanaweka maji, mchanga na vitu vingine ambavyo havifai kabisa ili kushusha ubora, ” alisema Ndimu.
Ofisa mwandamizi wa zao la pamba nchini, Emily Mbagulle, alisema ni jukumu la kila mdau wa zao la pamba, kuzingatia ubora wa zao hilo, kuanzia wakati wa kuandaa shamba, kulima, kuvuna, kuhifadhi, pamoja na wakati wa kuuza ili kuimarisha uboa wake.
“Hili ni jukumu letu sote kuhakikisha tunalinda na kuimaraisha ubora wa zao la pamba maana wote tunalitegemea zao hili,” alisema.
Akichangia hoja katika semina hiyo Meneja wa kiwanda cha Oram Tanzania LTD, Dick Chiriwo, kilichoko wilayani Bunda, aliwahasa wanunuzi wa zao hilo, kujenga mshikamano wa pamoja kwa kuacha kununua pamba ambayo haina ubora, kwa lengo la kupata pamba nyingi maana hiyo itakuwa ni hasara kwao.
“Wote wanunuzi mkishakamana na kukataa kabisa kununua pamba chafu mtakomesha hali hii….sasa unakuta mwingine anakataa kununua pamba chafu lakini mwingine wa sehemu hiyo hiyo anaikimbilia eti aweze kupata pamba nyingi, hiyo ni hasara kwenu acheni kabisa na wote mshikamane,” alisema Chiriwo.
Baadhi ya wanunuzi wa zao hilo wakiwemo wakulima na wanunuzi walisema kuwa kuna changamoto nyingi zinazowakabili wakulima, ikiwa ni pamoja na ya kutokupata pembejeo kwa wakati, pamoja na kupewa dawa za kuua wadudu ambazo hazina uwezo, pamoja na mbegu ambazo hazioti.