Thursday, 31 March 2016

Samatta: Tutaipiku Misri


Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta


NAHODHA wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta amesema Taifa Stars bado ina nafasi ya kufuzu fainali za Afrika (Afcon) mwakani.

Katika mawasiliano na gazeti hili kwa njia ya mtandao, Samatta anayecheza klabu ya KRC Genk iliyopo Ligi Kuu ya Ubelgiji, alisema amesikia kuhusu timu ya Taifa ya Misri kushinda mchezo wake dhidi ya Nigeria juzi na hivyo kufikisha pointi saba ambazo ndizo Tanzania inaweza kuzifikia ikishinda michezo yake miwili iliyobaki.

“Nimesikia Misri imeshinda bao 1-0 na sasa wana pointi saba, ukiangalia kwa juujuu unaweza kudhani wameshafuzu, lakini kiuhalisia bado, soka haipo hivyo. “Misri watakuja Dar es Salaam tunaweza kuwafunga kama walivyotufunga kwao (Misri iliifunga Taifa Stars mabao 3-0), pia mechi yetu ya Nigeria tukishinda tutakuwa nasi na pointi saba, tutashindana tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa,” alisema Samatta.

Kwa upande wake Mshauri wa Benchi la Ufundi la Taifa Stars, Abdallah Kibadeni, amesema Stars bado ina nafasi na kwamba matokeo ya Misri yasiwakatishe tamaa mashabiki.

Naye kocha wa zamani wa Ndanda FC ya Mtwara iliyopo Ligi Kuu Tanzania Bara, Ngawina Ngawina amesema mpira unadunda na kwamba dakika 90 za mchezo ndiyo zitaamua, hivyo Taifa Stars inaweza ikashinda mechi mbili ilizo nazo na ikafikisha pointi saba.

“Tuwape nafasi, tuwatie moyo wachezaji nina hakika tutafanikiwa. Fainali yetu ni Juni hapa wakija Misri tuwapige mabao mengi,” alisema.

Ngawina ambaye amepata kuchezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Juzi Misri iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Nigeria bao lililofungwa na Ramadan Sobhi Uwanja wa Borg El Arab mjini Cairo

Kutokana na matokeo hayo, Misri inaongoza Kundi G ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi mbili na Tanzania inashika nafasi ya mwisho ikiwa na pointi moja.

Kundi hilo limebaki na timu tatu tu, baada ya Chad kujitoa mwishoni mwa wiki, ambapo timu hiyo hadi inafikia uamuzi huo ilikuwa imefungwa mechi zake zote tatu ilizocheza.

Chad ilifungwa mabao 0-1 na Misri, mabao 2-0 na Nigeria na bao 1-0 na Tanzania. Misri itacheza na Taifa Stars Juni 4, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na baada ya mchezo huo, Stars itamaliza na Nigeria Septemba mwaka huu.

Yanga, Azam vitani leo



 
YANGA na Azam leo zinashuka kwenye viwanja tofauti katika michezo ya Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali.

Michuano hiyo inayojulikana pia kama Kombe la FA imeingia hatua ya robo fainali, ambapo Jumamosi iliyopita timu ya Mwadui iliifunga Geita Gold Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mabao 3-0 na kufuzu nusu fainali.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Yanga itacheza Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ikiwa mwenyeji wa Ndanda FC ya Mtwara, wakati Azam FC itakuwa Uwanja wa Azam Chamazi kuivaa Prisons.

Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) linatarajiwa kuendelea Alhamisi kwa michezo miwili kuchezwa katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo. Mechi zote zinatarajiwa kuwa na upinzani wa hali ya juu, huku kila timu ikipania kushinda na kufuzu nusu fainali.
Bingwa wa michuano hiyo atawakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) mwaka 2017.

Yanga na Azam pia zitatumia michezo hiyo kama maandalizi yao kwa ajili ya mechi za kimataifa mwishoni mwa wiki ijayo, ambapo Azam itacheza na Esperance ya Tunisia na Yanga itacheza na Al Ahly ya Misri.

Pia mechi ya leo ni maandalizi ya michezo ya viporo vya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo Yanga na Azam zitacheza kuanzia Jumamosi wiki hii. Robo fainali nyingine ya michuano hiyo itakuwa Aprili 9 mwaka huu, wakati Simba itakapokuwa mwenyeji wa Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wengine wakamatwa sakata la tumbili


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mtafungwa


SAKATA la kukamatwa kwa tumbili waliokuwa mbioni kusafirishwa nje ya nchi, limechukua sura mpya baada ya idadi ya waliokamatwa mpaka sasa kufikia watu saba wakiwemo maofisa wanne wa serikali.

Miongoni mwa waliokamatwa ni Ofisa Mfawidhi Kanda ya Kaskazini anayehusika na Matumizi Endelevu ya Wanyamapori nchini Nyangabo Musika, Idd Misanya anayedaiwa kuwauzia wanyama hao.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mtafungwa aliwataja watu hao kuwa ni Juma Eliasa ambaye ni Mkurugenzi wa Manyara Bird wakiunganishwa na raia wa Uholanzi waliokamatwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA, Arten Vardanian (52) na Edward Vardanian (46).

“Tumewakamata watu hawa na bado tunaendelea na mahojiano zaidi, uchunguzi utakapokamilika tutawafikisha mahakamani,” alisema Kamanda Mtafungwa.

Wakati kamatakamata hiyo ikiendelea, wafanyabiashara wanaohusika na uwindaji wa wanyama hao wanalalamikia kitendo cha kukamatwa kwa wageni hao kuwa kitaathiri biashara yao hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Nyara Kanda ya Kaskazini (TWEA), Athumani Bhoki alisema kuna mahala huenda waziri amepotoshwa kwani biashara hiyo ni halali na ina vibali vyote halali.

“Sisi hapa tuna vibali vilivyoidhinishwa kwa msimu aina ya wanyama na idadi yake kwa kampuni yangu ikiainishwa na ada ya malipo kwa serikali,” alisema Bhoki.

Alifafanua kuwa kwa tukio hilo litawashtua wateja wao wote kuwasiliana nao kwa ajili ya ununuzi wa wanyama hao kwa mwaka huu na kuwatia hasara kwani tayari wana idadi ya wanyama i wanawahifadhi na kuwatunza kwa ajili ya kupata masoko.

Naye Katibu wa chama hicho, Anthony Mushi alisema kwa tukio hilo, yeye tayari ana hasara kubwa kwani Waholanzi hao alikuwa na mkataba wa kuwauzia tumbili zaidi ya 174.

Aidha, alisema katika makubaliano hayo, baada ya mwezi mmoja wangefuata tena wanyama aina ya kima na tumbili zaidi ya 300 kwa kutumia usafiri wao ambayo ni fursa kubwa kibiashara.

Marekebisho sheria ya manunuzi kukabidhiwa Mwakyembe leo


Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe.



TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania leo itakabidhi taarifa ya utafiti wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011, Sura ya 410 kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe. Utafiti huo ulifanywa na Tume kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 8(1) na (2) cha Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria.

Ofisa Habari wa Tume hiyo, Munir Shemweta alisema mbali ya masharti ya kifungu hicho, pia taarifa hiyo ina hadidu za rejea zilizotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo aliitaka Tume kubainisha upungufu katika utekelezaji wa sheria na kubainisha madhara ya upungufu huo katika utekelezaji kwa serikali na taasisi zake.

Shemweta alisema katika utafiti Tume ilikutana na wadau mbalimbali kutoka Wizara, Idara,Taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali wakiwemo watalaamu waliobobea katika masuala ya ununuzi wa umma. Alisema taarifa ya Tume ina mapendekezo ya namna ya kuiboresha sheria hiyo ili ilete tija zaidi katika sekta ya ununuzi wa umma.

Utafiti wa sheria hiyo ulianza hivi karibuni ikiwa ni kuitikia agizo la Rais John Magufuli ambaye aliahidi kuifanyia marekebisho sheria hiyo wakati analizindua Bunge la 11 mwishoni mwa mwaka jana.

Akilihutubia Bunge katika eneo la kuziba mianya ya rushwa, Dk Magufuli aliahidi kuifumua sheria hiyo ambayo inatoa mianya kwa watumishi wa umma kuiba fedha za umma. “Tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ili kuhakikisha kwamba mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi hafifu tunaiziba” alisema Rais.

Japan yatoa bilioni 116/- Bajeti 2016/17


Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango.


SERIKALI imesaini hati mbili za makubaliano na Japan, yatakayoiwezesha Tanzania kupata Yen za Japan bilioni sita ambazo ni sawa na Sh bilioni 116.4 kwa ajili ya kusaidia kukamilisha bajeti ya mwaka 2016/2017.

Akizungumza wakati wa kutia saini na kubadilishana hati za makubaliano, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile alisema hati ya kwanza ya mkataba huo, ina lengo la kuboresha mazingira ya biashara nchini na kuongeza kasi ya uzalishaji wa ajira.

Alisema hati ya pili ni iliyosainiwa mwaka 1966 ya Wajapani waliokuwa wakija nchini kwa ajili ya kufanya shughuli za kujitolea, hivyo imerekebishwa kwa kuweka neno Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili waje kusaidia katika sekta za afya, elimu na sekta nyingine Tanzania Bara na Visiwani.

Aidha, Dk Likwelile alisisitiza kuwa kukosekana kwa fedha kutoka Marekani za Changamoto ya Milenia (MCC-2), hakutaathiri miradi iliyokuwa ikiendelea, ambayo ni pamoja na Mradi wa Umeme Vijijini (REA) kwa kuwa fedha hizo hazikujumuishwa katika bajeti.

“REA haiwezi kuathirika kwa sababu hizo fedha za MCC-2 hazikuwa kwenye bajeti, lakini tungeshukuru kama tungezipata kwa sababu zingeongeza uwezo na kufanya uboreshaji,” alisema Dk Likwelile.
Hata hivyo, aliwataka Watanzania kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika kuwezesha miradi ya maendeleo kwa kulipa kodi na kutoa taarifa juu ya wanaokwepa kodi ili nchi ijitegemee.

Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida alisema Serikali ya Japan itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kutengeza ajira hasa katika sekta binafsi kwa kupunguza gharama za kufanya biashara na kutengeza mazingira mazuri kwa viwanda.

“Serikali ya Japan ina nia ya dhati ya kuendelea kumuunga mkono Rais John Magufuli na serikali yake katika maono yake ya kujenga viwanda na kutengeneza ajira pamoja na kuwavutia wawekezaji wa kigeni kwa kutengeneza mazingira rafiki ya biashara,” alisema Balozi Yoshida.

Balozi Yoshida aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan unaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo na kwamba utasaidia kuongeza ukuaji wa uchumi na kijamii.

Wednesday, 30 March 2016

Mayanja: Akili yangu kwenye ubingwa tu




KOCHA Jackson Mayanja wa Simba, amewataka wadau kuacha kuangalia amekorofishana na nani, na badala yake waungane naye katika kufikiria maendeleo ya klabu huku akisema kwa sasa anachowaza ni ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alisema Simba kwa sasa inapambana kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo mawazo yote yako katika mbio hizo.

“Sina ugomvi na mtu hata mmoja, akili yangu ni kuhakikisha Simba inafanya vizuri kwa kushirikiana na wenzangu wote hadi uongozi. “Lakini kama atatokea mtu akafanya mambo ya utovu wa nidhamu, basi ajue hakutakuwa na mchezo, sitakubali,” alisema.

Mayanja aliingia kwenye mtafaruku na Hassan Isihaka ambaye alimjibu kocha huyo maneno yasiyo ya kiungwana. Baadaye akafuatia Abdi Banda na Mayanja amesisitiza wote kuadhibiwa, jambo ambalo limesifiwa sana na wadau wa soka kutokana na tabia yake ya kushikilia nidhamu.

Yanga kambini bila nyota tisa




Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi


IKIWA bila ya nyota wake tisa, wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga jana walianza kambi kujiandaa kwa michezo ya Kombe la FA, Ligi Kuu ya Tanzania Bara na ule wa kimataifa dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Iliingia kambini baada ya mazoezi ya asubuhi yaliyofanyika Uwanja wa Chuo cha Polisi Ufundi, Kurasini.

Akizungumza Dar es Salaam jana, kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema kikosi chake kimeingia kambini na wachezaji tisa ndio wanaokosekana, wakiwemo saba ambao ni wagonjwa na wengine wakiwa kwenye vikosi vyao vya timu za taifa.

Wanaoksekana katika kambi hiyo wametajwa kuwa ni Mbuyu Twite, Donald Ngoma, Malimi Basungu, Saidi Juma `Makapu’, Geofrey Mwashiuya, Simon Matheo na Benedicto Tinocco.


Tambwe na Niyonzima pia hawako kutokana na kukabiliwa na majukumu katika timu zao za taifa.
“Lakini wachezaji wetu wa kimataifa kama Amisi Tambwe (Burundi) na Haruna Niyonzima (Rwanda) hatutakuwa nao kwa vile wapo kwenye timu zao za taifa,” alisema Mwambusi.

Aliongeza kuwa, maandalizi yanaendelea vizuri huku akisema ari ya kikosi chake ni kubwa na dhamira ya uongozi ni kuona Yanga inafanya vizuri katika mashindano yote inayoshiriki.

“Tuna imani tutafanya vizuri kwani mpaka sasa tuna rekodi nzuri kwenye mashindano tunayoshiriki,” alisema bila kutaja mahali ilipo kambi yao, lakini ikiaminika ni moja ya hoteli za kifahari jijini Dar es Salaam.

Yanga wanaingia kambini wakijiandaa na wiki ngumu zaidi kwani, kwani watacheza mechi nne za mashindano matatu ndani ya siku 10.

Kesho wataanza kwa kumenyana na Ndanda FC ya Mtwara katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la FA, kabla ya kucheza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera Aprili 3 na dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro Aprili 6.

Siku tatu baadaye mabingwa hao wa soka nchini watamenyana na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.