JUMLA ya ng’ombe 22 wamekufa ghafla wakiwa wanachungwa katika kitongoji cha Kirumi Kijiji cha Tairo, Bunda mkoani Mara na kuleta hofu kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Ofisa Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, Rick Kaduri, tukio hilo limetokea Aprili 3 saa tisa mchana katika kitongoji hicho wakati ng’ombe hao wakichungwa na watoto wadogo.
Kaduri alisema ng’ombe waliokufa ni mali Mwita Masero mkazi wa kijiji cha Tairo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na thamani yake ni zaidi ya Sh milioni tisa.
Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mifugo hiyo imekufa kutokana na kula majani ambayo kiuhalisia huwa yana sumu kali, ambapo mifugo ikiyala kwa wingi hasa yanapoanza kuota upata madhara ya mfumo wa chakula tumboni na hatimaye kufa.
Aidha, Kaduri alitoa mwito kwa wananchi kufukia mizoga ya mifugo hiyo na kutokuthubutu kujaribu kula nyama ya ng’ombe wanaokufa ghafla.
Hata hivyo, alisema wamechukua sapuri ya vipimo ambavyo vitapelekwa kwa wataalamu wa mifugo na kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi juu ya vifo vya ng’ombe hao.
No comments:
Post a Comment