Wednesday, 5 April 2017

vifo vya ng'ombe vyaleta mtafaruku


















JUMLA ya ng’ombe 22 wamekufa ghafla wakiwa wanachungwa katika kitongoji cha Kirumi Kijiji cha Tairo, Bunda mkoani Mara na kuleta hofu kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Ofisa Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, Rick Kaduri, tukio hilo limetokea Aprili 3 saa tisa mchana katika kitongoji hicho wakati ng’ombe hao wakichungwa na watoto wadogo.
Kaduri alisema ng’ombe waliokufa ni mali Mwita Masero mkazi wa kijiji cha Tairo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na thamani yake ni zaidi ya Sh milioni tisa.
Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mifugo hiyo imekufa kutokana na kula majani ambayo kiuhalisia huwa yana sumu kali, ambapo mifugo ikiyala kwa wingi hasa yanapoanza kuota upata madhara ya mfumo wa chakula tumboni na hatimaye kufa.
Aidha, Kaduri alitoa mwito kwa wananchi kufukia mizoga ya mifugo hiyo na kutokuthubutu kujaribu kula nyama ya ng’ombe wanaokufa ghafla.
Hata hivyo, alisema wamechukua sapuri ya vipimo ambavyo vitapelekwa kwa wataalamu wa mifugo na kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi juu ya vifo vya ng’ombe hao.

Serengeti yaonja joto ya TRA


 


Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas









MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) jana ilishusha msafara wa timu ya taifa ya chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys na kukamata basi walilokuwa wakilitumia.
Serengeti ilikutana na zahama hiyo ikiwa nje ya kambi yao maeneo ya Kisutu Dar es Salaam tayari kwa safari ya kwenda kupata chakula cha jioni na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye aliwaalika kuwaaga.
Timu hiyo inayotarajiwa kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana mjini Gabon mwezi ujao, inatarajiwa kuondoka leo mchana kwenda Morocco kwa kambi ya maandalizi.
Akithibitisha taarifa hizo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema basi hilo ambalo hutumiwa na timu ya soka ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars lilikamatwa na kampuni ya udalali na minada ya Yono.
Takriban wiki tatu sasa, TRA imefunga ofisi na kuzuia baadhi ya mali za TFF kutokana na deni kubwa la malimbikizo ya kodi za mishahara ya aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Mbrazili Marcio Maximo kwa miaka minne tangu mwaka 2006- 2010.
Deni lingine linalosababisha ofisi za TFF kufungwa ni la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) la ziara ya timu ya taifa ya Brazil nchini mwaka 2010 ilipokuwa njiani kwenye Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia.