Wednesday, 5 April 2017

vifo vya ng'ombe vyaleta mtafaruku


















JUMLA ya ng’ombe 22 wamekufa ghafla wakiwa wanachungwa katika kitongoji cha Kirumi Kijiji cha Tairo, Bunda mkoani Mara na kuleta hofu kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Ofisa Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, Rick Kaduri, tukio hilo limetokea Aprili 3 saa tisa mchana katika kitongoji hicho wakati ng’ombe hao wakichungwa na watoto wadogo.
Kaduri alisema ng’ombe waliokufa ni mali Mwita Masero mkazi wa kijiji cha Tairo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na thamani yake ni zaidi ya Sh milioni tisa.
Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mifugo hiyo imekufa kutokana na kula majani ambayo kiuhalisia huwa yana sumu kali, ambapo mifugo ikiyala kwa wingi hasa yanapoanza kuota upata madhara ya mfumo wa chakula tumboni na hatimaye kufa.
Aidha, Kaduri alitoa mwito kwa wananchi kufukia mizoga ya mifugo hiyo na kutokuthubutu kujaribu kula nyama ya ng’ombe wanaokufa ghafla.
Hata hivyo, alisema wamechukua sapuri ya vipimo ambavyo vitapelekwa kwa wataalamu wa mifugo na kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi juu ya vifo vya ng’ombe hao.

Serengeti yaonja joto ya TRA


 


Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas









MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) jana ilishusha msafara wa timu ya taifa ya chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys na kukamata basi walilokuwa wakilitumia.
Serengeti ilikutana na zahama hiyo ikiwa nje ya kambi yao maeneo ya Kisutu Dar es Salaam tayari kwa safari ya kwenda kupata chakula cha jioni na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye aliwaalika kuwaaga.
Timu hiyo inayotarajiwa kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana mjini Gabon mwezi ujao, inatarajiwa kuondoka leo mchana kwenda Morocco kwa kambi ya maandalizi.
Akithibitisha taarifa hizo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema basi hilo ambalo hutumiwa na timu ya soka ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars lilikamatwa na kampuni ya udalali na minada ya Yono.
Takriban wiki tatu sasa, TRA imefunga ofisi na kuzuia baadhi ya mali za TFF kutokana na deni kubwa la malimbikizo ya kodi za mishahara ya aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Mbrazili Marcio Maximo kwa miaka minne tangu mwaka 2006- 2010.
Deni lingine linalosababisha ofisi za TFF kufungwa ni la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) la ziara ya timu ya taifa ya Brazil nchini mwaka 2010 ilipokuwa njiani kwenye Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Saturday, 4 February 2017

Makubwa zaidi yaibuka dawa za kulevya




SIKU moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutangaza vita dhidi ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, makubwa zaidi yamezidi kujitokeza baada ya orodha ya watu hao wanaojihusisha na biashara hiyo haramu kuongezeka.
Mkuu huyo wa mkoa amemuagiza Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro kuwaongeza askari wengine watatu katika orodha ya watuhumiwa hao ambao alidai katika wiki mbili zilizopita walipewa Sh bilioni moja kutokana na biashara hiyo.
Aliwataja askari hao kuwa ni Muddy Zungu, Fadhili na Ben huku wengine wanaopaswa kuongezwa katika orodha hiyo ni pamoja na msanii Vanesa Mdee na Video Queen, Tunda Sebastian.
Aidha, Makonda alimuagiza Sirro kuhakikisha wasanii na watu wengine walioko kwenye orodha aliyoitaja awali ambao hawakufika, wakamatwe mara moja na wawekwe ndani hadi Jumatatu kwa ajili ya mahojiano.
“Hawa nataka waunganishwe na wale wenzao, hatuwezi kuwa na watumishi wanaochafua taaswira ya jeshi la polisi na nimepata taarifa mmoja amenunua nyumba Kigamboni,” alisema Makonda.
Makonda pia alimtaja mtu mwingine ambaye ni mfanyabiashara mkubwa wa dawa hizo, Omari Sanga kuwa ni mmoja kati wa watu waliosababisha asilimia 65 hadi 70 ya Watanzania waishie kwenye jela nchini China.
Pia aliitaja hoteli ya Meditteranian iliyopo Kawe kuwa nayo ni miongoni mwa hoteli ambazo zimekuwa zikifanya biashara hiyo kinyume na leseni waliyopewa.
Watuhumiwa waliofika ni pamoja na aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Wema Sepetu, Khaleed Mohammed (TID), Hamidu Chambuso (Dogo Hamidu/ Nyandu Tozzy) pamoja na Babuu wa Kitaa.

Thursday, 27 October 2016

Mourinho ashtakiwa na FA kwa kumuingilia refa

  • Mshirikishe mwenzako

Jose Mourinho
Image captionJose Mourinho

Mkufunzi wa Manchester United Jose Mourinho ameshtakiwa na shirikisho la soka nchini Uingereza FA kwa kudai kwamba itakuwa vigumu kwa refa Anthony Taylor kusimamia mechi yao dhidi ya Liverpool.
Mourinho aliongezeawamba kumteua Taylor kusimamia mechi hiyo ya tarehe 16 Oktoba ilimpatia shinikizo refa huyo mwenye makao yake Manchester.
Mameneja hawaruhusiwa kuzungumzia kuhusu marefa kabla ya mechi.
Mourinho ana hadi Oktoba 31 kujibu shtaka la ukosefu wa nidhamu na kusababisha mechi hiyo kuwa na jina baya.
Taylor alito kadi 4 za njano zote kwa timu ya Manchester United katika sare hiyo ya 0-0

Monday, 25 July 2016

Rais Magufuli mgeni rasmi Sherehe za Mashujaa Dodoma



AMIRI Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Kitaifa, yatakayofanyika mjini Dodoma leo.

Hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa maadhimisho hayo kufanyika nje ya Jiji la Dar es Salaam, tangu Tanzania ipate Uhuru wake mwaka 1961. 

Pia, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuongoza maadhimisho hayo tangu alipochaguliwa Oktoba mwaka jana.

"Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yatafanyika kitaifa mkoani Dodoma katika Uwanja wa Mashujaa siku ya Jumatatu (leo) Julai 25, 2016 kuanzia saa 1 kamili asubuhi hadi saa 4:30 asubuhi. 

“Mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli," alisema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, jana.

Alisema anaishukuru serikali kwa kuupatia mkoa huo, ambao ni Makao Makuu ya nchi, heshima ya kipekee katika historia ya nchi ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kitaifa.

Rugimbana alitaja shughuli zitakazofanyika siku hiyo kuwa ni gwaride la maombolezo litakaloshirikisha vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na Magereza.

Kutakuwa pia na upigaji mizinga na uwekaji wa silaha za asili na shada la maua kwenye mnara, kama ishara ya kumbukumbu kwa mashujaa. Shughuli nyingine ni utoaji wa dua na sala, utakaofanywa na viongozi wa madhehebu ya dini.

Rugimbana aliwataka wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwenye Viwanja vya Mashujaa kushiriki kwenye maadhimisho hayo. Alisema hadi jana, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya shughuli hiyo yalikuwa yamekamilika.